Fasihi Grade 7 & 8 Lesson Notes
CHIMBUKO NA DANA ZA FASIHI
Maana ya Fasihi: Fasihi ni sanaa ya lugha inayotumia lugha kutoa na kuwasilisha sanaa mbalimbali katika jamii.
Tanzu Kuu za Fasihi:
Fasihi Simulizi: Fasihi inayowasilishwa kwa njia ya mdomo na/au matendo.
Hadithi (Ngano): Hekaya, mighani, visasili, n.k.
Nyimbo: Nyimbo za jandoni, za ndoa, za kazi (hodiya/wawe), za kidini, bembelezi, na za watoto.
Maigizo: Michezo ya kuigiza, ngomezi, n.k.
Tungo Fupi: Methali, vitendawili, misemo, n.k.
Fasihi Andishi: Fasihi inayowasilishwa kwa njia ya maandishi.
Hadithi Fupi: Hadithi isiyokuwa ndefu iliyochapishwa katika mkusanyiko wa hadithi nyingine.
Riwaya: Hadithi ndefu iliyochapishwa katika kitabu chake pekee.
Tamthilia: Mchezo wa kuigiza uliowekwa kwa njia ya maandishi.
Ushairi: Mashairi yaliyoandikwa na kuchapishwa.
Tanbihi Kuhusu Ushairi: Ushairi unaweza kuwa kipera cha nyimbo katika Fasihi Simulizi, lakini pia unaweza kuwa chini ya Fasihi Andishi ikiwa umechapishwa kwenye vitabu au maandishi.
Tofauti kati ya Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi:
Fasihi Simulizi | Fasihi Andishi |
|---|---|
1. Huwasilishwa kwa njia ya mdomo na/au matendo. | 1. Huwasilishwa kwa njia ya maandishi. |
2. Ni mali ya jamii nzima. | 2. Ni mali ya mwandishi (na mchapishaji). |
3. Msimulizi anaweza kubadilisha sehemu fulani kulingana na mahitaji. | 3. Kitabu kilichoandikwa hakiwezi kubadilishwa kirahisi. |
4. Huhifadhiwa akilini / kichwani. | 4. Huhifadhiwa vitabuni, kwenye kanda za sauti au filamu. |
5. Kazi simulizi hubadilika kulingana na wakati na mazingira. | 5. Kazi andishi haibadiliki na wakati. |
6. Huhitaji msimulizi na hadhira wawe mahali pamoja wakati wa masimulizi. | 6. Msomaji anaweza kusoma peke yake, mahali popote na wakati wowote. |
7. Mtu yeyote anaweza kutunga na kusimulia bila hitaji la kujua kusoma. | 7. Ni lazima mwandishi na msomaji wawe na uwezo wa kusoma na kuandika. |
8. Hutumia wahusika changamano (wanyama, watu, mazimwi, viumbe visivyo na uhai, n.k.). | 8. Hutumia wahusika wanadamu zaidi. |
SIFA NA UMUHIMU WA FASIHI
Sifa za Fasihi Simulizi:
Utendaji: Huwa na vitendo halisi vinavyoshirikisha fanani na hadhira kwa wakati mmoja.
Uwepo wa Fanani na Hadhira: Hukutanisha mtambaji na wasikilizaji/watazamaji mahali pamoja. Fanani huweza kusimulia, kupiga makofi, au kubadilisha miondoko; hadhira hushiriki kwa kuuliza maswali, kupiga makofi, kuimba, na kushangilia.
Njia ya Mzungumzo: Huwasilishwa kwa njia ya mdomo.
Kuhifadhiwa Akilini: Asili yake ni kuhifadhiwa kichwani na kurithishwa kizazi hadi kizazi kwa njia ya mdomo.
Uhuru wa Msanii: Msimulizi ana uhuru wa kufanya mabadiliko kulingana na rika, wakati, na mazingira bila ugumu.
Umiliki wa Jamii: Kazi ya fasihi simulizi ni mali ya jamii nzima.
Wakati na Pahala Maalum: Huwa na nyakati na mahali maalum pa kuiwasilisha (mfano: ngano jioni motoni).
Matumizi ya Viungo vya Mwili: Huruhusu matumizi ya ishara-uso, mikono, na viungo vingine vya mwili wakati wa uwasilishaji.
Sifa za Fasihi Andishi:
Maandishi: Huwasilishwa katika mfumo wa maandishi.
Uthabiti wa Maudhui: Haipokei mabadiliko ya papo kwa papo; ikishaandikwa haibadiliki hadi toleo jingine lichapishwe.
Mawasiliano ya Upande Mmoja: Mwandishi hawani moja kwa moja na msomaji wakati wa usomaji.
Umiliki wa Mtu Binfasi: Mtunzi halisi anajulikana na kazi ni mali yake.
Hifadhi ya Kudumu: Huhifadhiwa kwa maandishi, kanda za sauti, au filamu.
Uthabiti wa Sanaa: Si rahisi kupoteza muundo au sanaa yake ya awali.
Umuhimu wa Fasihi Katika Jamii:
Kuburudisha: Kutumbuiza, kufurahisha, na kusisimua hadhira.
Kuelimisha: Kutoa elimu kuhusu jamii, mazingira, historia, na maisha.
Kudumisha Maadili: Kuelekeza, kuonya, na kunasihi jamii kuhusu tabia zinazokubalika.
Kuunganisha Jamii: Kukuza ushirikiano kupitia nyimbo, miviga, na vichekesho.
Kukuza Lugha: Kutumia mbinu mbalimbali za lugha na kukuza ukwasi wa msamiati.
Kuhifadhi Tamaduni: Kuhifadhi mila, desturi, na itikadi za jamii.
Kukuza Uwezo wa Kufikiri: Kuchochea akili ya hadhira kupitia vipera kama vitendawili na ngano za mtanziko.
NYIMBO KATIKA FASIHI SIMULIZI
Maana ya Nyimbo: Ni aina ya sanaa katika fasihi inayotumia lugha teule, sauti, na kiimbo maalum. Mara nyingi huendamana na ala za muziki kama vile ngoma na hugawanywa katika beti na mishororo, huku ikijumuisha kiitikio kinachorudiwarudiwa.
Sifa za Nyimbo:
Hutumia kiimbo au sauti maalum.
Huweza kuendamana na ala za muziki.
Huimbwa na mtu mmoja au watu wengi (peke yake au kwa kupokezanwa).
Hutumia lugha ya mkato.
Hurudiarudia (kukariri) maneno ili kusisitiza ujumbe.
Umuhimu wa Nyimbo:
Kuburudisha jamii.
Kuelimisha, kufunza, kuonya, na kuelekeza.
Kuliwaza wakati wa huzuni au taabu.
Kusifia mtu au kitu katika jamii.
Kuunganisha jamii.
Kudumisha na kuhifadhi tamaduni za jamii.
Kukuza talanta na sanaa.
Kutumika kama mbinu ya uwasilishaji katika tanzu zingine (mfano: ndani ya ngano).
Aina za Nyimbo Kulingana na Ujumbe/Maudhui:
Hodiya / Wawe (Nyimbo za Kazi):
Maana: Nyimbo zinazoimbwa na watu wanapofanya kazi ili kutia bidii na kuondoa uchovu.
Sifa: Huimbwa kazini (ukulima, uwindaji, uvuvi); huimbwa na mtu mmoja au kundi; zina maneno ya kuhimiza; urefu na mdundo hutegemea kasi na aina ya kazi.
Majukumu: Kuburudisha wafanyikazi, kurahisisha kazi kwa kupunguza mawazo ya uchovu, kuhimiza bidii na kuwanya watu wapende kazi zao.
Nyimbo za Kidini:
Maana: Nyimbo zinazoimbwa kumsifia Mungu, kuomba, au kutoa mafunzo ya kiroho.
Sifa: Hutumia kiimbo maalum, huandamana na ala za muziki, huimbwa na mtu mmoja au wengi, na hutumia lugha ya mkato pamoja na urudiaji.
Nyimbo za Bembelezi (Lullabies):
Maana: Nyimbo zinazoimbwa kumbembeleza mtoto aache kulia au alale.
Sifa: Huimbwa na akina mama au walezi; ni fupi; huimbwa kwa sauti ya chini, nyororo na ya taratibu; zina mahadhi mazuri; huimbwa mtoto akiwa amebebwa au kutumbuizwa; zina urudiaji wa kibwagizo na lugha ya kushawishi (kutoa ahadi ya zawadi).
Majukumu: Kunyamazisha mtoto, kuwaongoa watoto walale, kutumbuiza, kusuta wasiopa watoto malezi bora, na kuonya mtoto dhidi ya tabia mbaya kama kulia ovyo.
Nyimbo za Watoto:
Maana: Nyimbo zinazoimbwa na watoto wakiwa mchezoni au katika shughuli zao.
Sifa: Zina urudiaji wa vifungu, huwasilishwa na watoto wenyewe, huandamana na michezo au kuchesha viungo vya mwili, na hutumia mafungu mafupi ya maneno.
Majukumu: Kuburudisha, kuelimisha watoto kuhusu jamii, kukuza umoja na ushirikiano, na kukashifu tabia hasi kama vile uchoyo na ugomvi.
Wahusika na Vipengele vya Lugha Katika Nyimbo:
Wahusika: Mwimbaji na Hadhira lengwa.
Mbinu za Lugha:
Urudiaji wa maneno: Kusisitiza ujumbe.
Nahau: Maneno yenye maana maalum isiyotokana na maana ya kawaida ya maneno hayo.
Mfano: Amekula chumvi nyingi - Ameishi miaka mingi.
Mfano: Ahadi ni deni - Timiza ahadi yako.
Methali: Misemo ya hekima yenye maana iliyofumbwa.
Maneno yasiyokuwa na maana ya msamiati: Kutumika kukamilisha mdundo au urari wa sauti.
USHAIRI NA UCHAMBUZI WAKE
Maana ya Ushairi: Ushairi ni utungo wa kisanaa unaotumia lugha teule na mpangilio maalum wa maneno (badala ya lugha natharia/ya mfululizo) ili kupitisha ujumbe. Mashairi yanayoghanwa badala ya kuimbwa huitwa maghani.
Aina za Mashairi Kulingana na Idadi ya Mishororo Katika Kila Ubeti:
Umoja / Tathmina: Shairi lenye mshororo mmoja (1) katika kila ubeti.
Tathnia: Shairi lenye mishororo miwili (2) katika kila ubeti.
Tathlitha: Shairi lenye mishororo mitatu (3) katika kila ubeti.
Tarbia: Shairi lenye mishororo minne (4) katika kila ubeti. (Hii ndiyo aina inayotumiwa zaidi).
Takhmisa: Shairi lenye mishororo mitano (5) katika kila ubeti.
Tasdisa: Shairi lenye mishororo sita (6) katika kila ubeti.
Usaba: Shairi lenye mishororo saba (7) katika kila ubeti.
Ukumi: Shairi lenye mishororo kumi (10) katika kila ubeti.
Bahari za Ushairi (Kulingana na Muundo, Vina, Mizani, na Vipande):
Utenzi: Shairi refu lenye kipande kimoja tu katika kila mshororo.
Mathnawi: Shairi lenye vipande viwili (ukwapi na utao) katika kila mshororo.
Mfano: Ewe mtunga silabi, na sauti ya kinubi, Majukumu hatubebi, maadamu hatushibi, Mateso kwa ajinabi, kwa mabwana na mabibi Ukija hayatukabi, karibia karibia
Ukawafi: Shairi lenye vipande vitatu (ukwapi, utao, na mwandamo) katika kila mshororo.
Mfano: Nashindwa nikupe nini, nishukuru kwa malezi, mapenzi na riziki, Ni pendo kiasi gani, lishindalo la mzazi, kweli mama hulipiki, Ulinilinda tumboni, ukilemewa na kazi, ila moyo huvunjiki, Kanilisha utotoni, mavazi pia malazi, ukitafuta kwa dhiki.
Mavue: Shairi lenye vipande vinne (ukwapi, utao, mwandamo, na ukingo) katika kila mshororo.
Mfano: Sisi walipa ushuru, wajenga taifa, tena kwa bidii, twahangaishwa, Tumenyimwa uhuru, tuna mbaya sifa, hatujivunii, tunapopotoshwa, Kila tunapopazuru, damu na maafa, hatutulii, hali ya kutishwa
Ukaraguni: Shairi ambalo vina vyake vya kati na vya mwisho hubadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
Ukara: Shairi ambalo vina vya kipande kimoja havibadiliki kutoka ubeti mmoja hadi mwingine, lakini vina vya kipande kingine vinabadilika (mfano: vina vya kati vinafanana kote lakini vya mwisho vinabadilika).
Mtiririko: Shairi ambalo vina vyake vya kati na vya mwisho havibadiliki kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho.
Mkufu / Pindu: Shairi ambalo neno la mwisho au kifungu cha mwisho cha ubeti mmoja hutangulia katika mshororo wa kwanza wa ubeti unaofuatia.
Mfano: …Bali twaisikiliza, bila ya kuzungumza, Bila ya kuzungumza, wala mwendo kulegeza…
Kikwamba: Neno moja au kifungu cha maneno kurudiwarudiwa kuanzia mishororo au beti za shairi.
Mfano: Jiwe hili lala nini, ila moshi na majani, Jiwe linalala lini, litokapo vileoni, Jiwe hili halineni, lina macho halioni, Jiwe na tulibebeni, tulitupe mitaroni
Kikai: Shairi lenye kipande kimoja kifupi chenye mizani chache kuliko kingine (mfano: mizani 8, 4).
Mfano: Nani binadamu yule, adumuye, Anayeishi milele, maishaye
Msuko: Shairi ambalo kibwagizo au mshororo wake wa mwisho ni mfupi kuliko mishororo mingine ya ubeti (mfano: 8,8; 8,8; 8,8; 8).
Mfano: Hawajazawa warembo, usidhani umefika, Ukisifiwa mapambo, jinsi ulivyoumbika, Akipata jipya umbo, 'tabaki kihangaika, Usidhani umefika.
Mandhuma: Shairi ambalo kipande kimoja hutoa wazo au swali, na kipande cha pili kikitoa jibu au suluhisho.
Malumbano: Mashairi mawili ambapo washairi wawili wanajibizana au kupingana kitunzi.
Ngonjera: Shairi lenye wahusika wawili au zaidi wanaojibizana (mfano: ubeti wa kwanza mwalimu, wa pili mwanafunzi).
Sakarani: Shairi lililochanganya bahari zaidi ya moja.
Sabilia: Shairi lisilokuwa na kibwagizo (mshororo wa mwisho unabadilika kutoka ubeti hadi ubeti).
Shairi Huru: Shairi lisilozingatia sheria za kiarudhi za ushairi wa jadi.
Shairi Guni: Shairi lenye makosa ya kiarudhi (kama vile kuvunjika kwa mizani au urari wa vina).
Mambo Muhimu Katika Uchambuzi wa Mashairi:
Muundo / Umbo: Idadi ya mishororo katika kila ubeti, idadi ya mizani katika kila mshororo na kipande, idadi ya vipande, kituo/kibwagizo/kiishio, na urari wa vina.
Uhuru wa Mshairi (Kuvunja Sheria za Kisarufi):
Inkisari: Kupunguza idadi ya silabi katika neno ili kutosheleza mizani (mfano: nimeona kuwa meona; aliyenipenda kuwa alenipenda).
Mazda: Kuongeza silabi katika neno ili kutimiza idadi ya mizani (mfano: afya kuwa afiya).
Tabdila: Kubadilisha silabi ya mwisho ya neno ili kupata urari wa vina bila kuathiri mizani (mfano: dunia kuwa duniya).
Kuboronga Sarufi: Kubadilisha mpangilio wa kawaida wa maneno katika sentensi ili kupata urari wa vina au mdundo (mfano: siku hiyo ikifika kuwa ikifika hiyo siku).
Utohozi: Kuswahilisha maneno kutoka lugha ngeni ili kudumisha mdundo wa kishairi (mfano: intaneti badala ya internet).
Maudhui: Ujumbe na mawazo mbalimbali yanayojitokeza kwenye shairi.
Dhamira: Lengo, dhumuni, au nia ya mshairi (mfano: kuonya, kutahadharisha, au kunasihi).
Mtindo wa Lugha: Mbinu za kisanaa alizotumia mshairi (tanakali za sauti, istiara, takriri, semi, n.k.).
Istilahi za Kishairi:
Shairi: Sanaa ya maneno inayotumia mpangilio na uteuzi maalum wa maneno na sauti ili kupitisha ujumbe.
Vina: Silabi za mwisho katika kila kipande cha mshororo.
Mizani: Idadi ya silabi katika kila mshororo.
Mshororo: Msitari mmoja wa maneno katika shairi.
Ubeti: Kifungu cha mishororo kadhaa katika shairi.
Vipande: Visehemu vya mshororo vilivyotenganishwa kwa alama ya kituo (,).
Ukwapi: Kipande cha kwanza katika mshororo.
Utao: Kipande cha pili katika mshororo.
Mwandamo: Kipande cha tatu katika mshororo.
Ukingo: Kipande cha nne katika mshororo.
Mwanzo: Mshororo wa kwanza katika ubeti.
Mloto: Mshororo wa pili katika ubeti.
Kimalizio / Kiishio: Mshororo wa mwisho katika ubeti ambao haurudiwirudiwi katika beti zingine.
Kibwagizo: Mshororo wa mwisho katika ubeti unaorudiwarudiwa katika kila ubeti.
Sifa za Ushairi:
Huwa na vina, mizani, mishororo, na beti.
Hutumia lugha teule na ya mkato.
Hufupisha au kurefusha maneno ili kutosheleza mizani.
Huwa na uhuru wa mshairi unaokiuka kanuni za kisarufi.
Hutumia mbinu mbalimbali za lugha.
Umuhimu wa Mashairi: Kuburudisha, kuhamasisha jamii, kukuza sanaa na ukwasi wa lugha, kuliwaza, kuelimisha, kuonya/kutahadharisha, kupitisha ujumbe, kusifia, na kukejeli au kukemea mambo yanayoenda kinyume na maadili.
MIGHANI AU VISAKALE
Maana ya Mighani (Visakale): Ni hadithi za mashujaa (majagina) wanaosifiwa katika jamii kwa kupigania jamii zao katika vita vya ukombozi au dhidi ya maadui (majahili).
Sifa za Mighani:
Hutumia mbinu ya chuku (mubalagha) kusifia matendo na uwezo wa shujaa.
Shujaa huwa na uwezo wa ukiamaumbile (uwezo unaozidi wa binadamu wa kawaida).
Ni vigumu sana kwa shujaa kuuawa licha ya wingi wa maadui.
Shujaa huwa na siri kuu ya nguvu zake (mfano: nguvu kuwa kwenye kivuli, nywele, kitovu, n.k.).
Shujaa hupigania haki na ukombozi wa jamii yake.
Jamii ya shujaa huwakilisha wema ilhali maadui huwakilisha ubaya.
Jagina hufa mwishoni mwa hadithi, hasa baada ya kusalitiwa na mtu wa karibu.
Huaminika na jamii kuwa za kweli au zenye msingi wa kihistoria.
Sifa za Jagina (Shujaa):
Huwa na nguvu zinazotokana na siri maalum.
Ana uwezo wa ukiamaumbile.
Hupigania haki za jamii yake.
Huwa na kimo kisichokuwa cha kawaida (mfano: mfupi sana au mrefu sana).
Ni mtu mwema kulingana na maadili ya jamii yake.
Umuhimu wa Visakale: Kuunganisha jamii, kuhifadhi historia ya jamii, kuelimisha na kunasihi, na kuburudisha.
Majagina Maarufu na Muktadha Wao:
Jagina (Shujaa) | Kabila / Jamii | Muktadha / Mambo Aliyofanya |
|---|---|---|
Mekatilili wa Menza | Giriama | Mwanamke aliyeongoza jamii dhidi ya wakoloni. |
Fumo wa Linyongo | Wapate | Alipigana vita dhidi ya Sultani wa Pate. |
Kinjeketile Ngwale | Wamatumbi | Aliyeongoza Vita vya Majimaji. |
Luanda Magere | Luo | Alipigana vita dhidi ya Wanandi (nguvu zake zilikuwa kwenye kivuli). |
Koitalel arap Samoei | Nandi | Aliyeongoza Vita vya Nandi Rebellion dhidi ya wakoloni. |
Shaka | Zulu | Mfalme aliyepanua na kuongeza ufalme wa Kizulu. |
Vipengele vya Kuzingatia Katika Kuwasilisha Mighani: Matumizi ya lugha kulingana na hadhira, kuhusisha hadhira, kutumia maswali ya balagha, na matumizi ya tamathali za semi (chuku, urudiaji, n.k.).
HADITHI ZA FASIHI SIMULIZI
a. Visasili:
Maana: Ngano za kihistoria zinazoeleza chimbuko au asili ya jamii/kabila fulani, tamaduni zao, na jinsi walivyofika katika eneo lao la sasa. Hueleza mambo yasiyoelezeka kwa urahisi kama vile kifo, jando, tohara, na ndoa.
Tofauti kati ya Visasili na Usuli (Visaviini): Visasili huhusisha jamii fulani, mila, imani, na matukio ya kiada (kifo, tohara); ilhali ngano za usuli huelezea kwa nini mambo fulani ya kimaumbile hufanyika bila kuhusisha jamii au imani mahsusi.
Sifa za Visasili: Huelezea chimbuko la jamii; matukio yake yalitokea zamani sana (mwanzoni mwa dunia); huhusisha miungu au malaika; na huburudisha.
Umuhimu: Kutafuta majibu kwa maswali yanayotatiza, kuhifadhi historia na imani, kuunganisha jamii, na kuwasilisha mila na desturi.
Mifano: Asili ya jamii ya Wamaasai, Asili ya Wagikuyu.
Uwasilishaji: Kuchagua wahusika wanaofaa, matumizi ya lugha kulingana na hadhira, kuhusisha hadhira, na kupitisha ujumbe mahususi.
b. Hurafa / Khurafa:
Maana: Hadithi ambazo wahusika wake wote ni wanyama wanaopewa uwezo wa kibinadamu (kuongea, kufikiri, kufanya kazi) ili kuangazia na kutoa funzo kuhusu tabia za kibinadamu.
Tanbihi: Kwa kuwa wahusika wote ni wanyama tangu mwanzo hadi mwisho, mbinu ya tashihisi/uhuishaji haitumiwi kama mbinu ya sanaa bali ni muundo wa utanzu wenyewe.
Sifa: Wahusika ni wanyama wenye uwezo wa kibinadamu; hurejelea masuala ya kijamii (uongozi, uchumi, utangamano); na funzo lake huwa wazi (mfano: kukanya tamaa au ujinga).
Umuhimu: Kuburudisha, kuelimisha watoto kuhusu wanyama na sifa zao, kukuza maadili, kuelekeza na kunasihi.
Wanyama na Sifa Zao Katika Hurafa:
Sungura: Mjanja na mwerevu; huwakilisha watu wanaotumia ujanja kula jasho la wengine au kushinda maadui.
Simba: Kiongozi au mfalme; huwakilisha watu wakali na wenye mamlaka wanaoogopwa katika jamii.
Fisi: Mlafi na mwenye tamaa; huwakilisha wanadamu wazembe, wajinga, na wasiofikiri kwa kina.
Nyani: Mwenye hekima; hutumika kama hakimu au kiongozi mwenye busara.
Nyoka: Mwenye hila na ulaghai katika jamii.
Kobe: Mpole, mnyamavu, na mwenye subira; mwishowe huibuka mshindi.
Ndovu: Mwenye kimbelembele, kujisifu, na kujitafutia umaarufu bila ujuzi wa kutosha.
c. Hekaya:
Maana: Hadithi zenye mhusika mmoja mjanja au mwerevu kuliko wenzake, anayetumia ujanja huo kujinufaisha kutoka kwa wengine wanaodanganyika kwa urahisi.
Sifa: Huwa na mhusika mjanja anayehadaa wenzake; mhusika huyo hunufaika hata kama hastahili; ni fupi na ina funzo mahsusi.
Umuhimu: Kuburudisha, kutoa mafunzo, kutahadharisha, na kuelekeza.
Mifano: Hadithi za Abunuwasi, Hadithi za Sungura na Fisi.
Tofauti Kati ya Mighani na Visasili:
Mighani | Visasili |
|---|---|
Husimulia kuhusu mashujaa na vita vyao. | Husimulia historia na chimbuko la jamii. |
Wahusika wakuu ni majagina. | Wahusika ni binadamu, miungu, wanyama, n.k. |
Hueleza sifa na matendo ya ukiamaumbile ya majagina. | Husimulia asili ya vitu, mianzo ya desturi, na mila. |
TAMTHILIA NA WAHUSIKA KATIKA FASIHI ANDISHI
Maana ya Tamthilia: Ni sanaa inayowasilisha mchezo wa kuigiza kwa njia ya maandishi. Majina ya wahusika huandikwa upande wa kushoto, yakifuatiwa na koloni (:), kisha maneno halisi yaliyotamkwa.
Vipengele vya Kuhakiki Tamthilia:
Maudhui: Jumla ya mawazo na ujumbe unaozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo.
Dhamira: Lengo au dhumuni kuu la mwandishi. Kuna Dhamira Kuu (kiini cha kazi/wazo kuu) na Dhamira Ndogondogo (mawazo madogo yanayojenga dhamira kuu).
Aina za Wahusika Katika Fasihi Andishi:
Wahusika Wakuu: Wahusika wanaojitokeza kutoka mwanzo hadi mwisho na kuhusishwa na visa takribani vyote.
Wahusika Wasaidizi: Wahusika wanaosaidia kujenga na kukuza sifa za mhusika mkuu (mfano: marafiki au familia).
Wahusika Wadogo: Wahusika wenye majukumu madogo kama vile kujenga mandhari au maudhui madogo (wakitolewa kazi haiharibiki sana).
Wahusika Bapa: Wahusika wasiobadilika kitabia tangu mwanzo hadi mwisho.
Bapa-sugu: Wanaonyesha msimamo wao thabiti kulingana na masimulizi.
Bapa-vielelezo: Msimamo wao unatambulika kupitia majina yao ya majazi (mfano: mhusika Rehema kuwa mwenye huruma kote).
Wahusika Duara: Wahusika wanaobadilika kitabia kulingana na hali, mazingira, au maudhui (hawana msimamo mmoja).
Wahusika Wafoili: Wahusika walioko katikati ya bapa na duara; wanaweza kuchukua msimamo fulani lakini wakabadilika baadaye kulingana na wahusika wanaotangamana nao.
VIPENGELE VYA LUGHA KATIKA HADITHI
Sitiari / Istiari: Kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo 'ni' au 'kuwa'.
Tashbiha: Kulinganisha vitu au hali mbili kwa kutumia maneno ya mfananisho kama kama, mithili ya, sawa na, ja.
Takriri: Kurudiarudia neno au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe.
Tashihisi / Uhuishaji: Kupatia kitu kisicho na uhai sifa za kiumbe mwenye uhai (sifa za kibinadamu).
Methali: Misemo ya hekima yenye maana iliyofumbwa inayotumiwa kupitisha ujumbe mzito.
Semi: Ungo la maneno linalotoa maana tofauti na maana ya kawaida ya maneno hayo. Ziko za aina mbili: Nahau (zina vitenzi) na Misemo (haina vitenzi).
Tanakali za Sauti: Mbinu ya kuiga sauti, mliyo, au namna kitendo kilivyofanyika.
Maswali ya Balagha (Tashititi): Maswali yanayoulizwa na msimulizi/mhusika asiyotarajia jibu kwani jibu lake liko wazi.
Uzungumzi Nafsiya: Mhusika kujizungumzia mwenyewe au kuwaza moyoni bila kukusudia kusikiwa na wengine.
Kinaya: Hali au matukio kuwa kinyume kabisa na matarajio ya kawaida ya hadhira.
Kejeli: Mbinu ya kutumia maneno ya dharau au kejeli ili kukemea au kudhalilisha kitendo/mtu.
Taharuki: Hali ya kuacha hadhira na hamu kubwa ya kutaka kujua kilichotokea au kitakachotokea baadaye.
Sadfa: Matukio viwili vinavyohusiana kukutana au kutokea kwa wakati mmoja kana kwamba vilipangwa, ingawa havikupangwa.
Kisengere Nyuma (Mbinu Rejeshi / Flashback): Mwandishi kurudi nyuma katika wakati na kusimulia kisa kilichotokea awali.
Kisengere Mbele (Utabiri / Foreshadowing): Mwandishi kubadilisha wakati na kusimulia au kutabiri mambo yatakayotokea siku za usoni.
Njozi / Ndoto: Kutumia ndoto kutabiri yatakayojiri au kufumbua jambo lililokuwa fumbo.
FANANI NA HADHIRA KATIKA FASIHI SIMULIZI
Sifa za Mtambaji wa Hadithi (Fanani / Mganaji):
Mchangamfu na mcheshi ili kuvutia hadhira.
Anafahamu utamaduni wa jamii yake kwa kina.
Anaifahamu hadhira yake vizuri na kusimulia kulingana na rika zao (watoto, vijana, wazee).
Ana uwezo wa ufaraguni (kuchomekea na kubadilisha sehemu za sanaa papo kwa papo).
Mwenye kumbukumbu nzuri.
Ana uwezo wa kuigiza kwa kutumia viungo vya mwili, ishara-uso, na mabadiliko ya sauti (kiimbo).
Ana uwezo wa kujenga taharuki kwa kusita kidogo.
Anashirikisha hadhira katika nyimbo na michezo.
Ni mlumbi hodari na mkwasi wa lugha.
Aina za Hadhira:
Hadhira Tendi / Hai: Hadhira inayoshiriki kikamilifu kwa kuimba, kujibu maswali, kupiga makofi, na kutazama.
Hadhira Tuli: Hadhira inayosikiliza au kutazama tu bila kuchangia moja kwa moja wakati wa uwasilishaji.
Aina za Wahusika Katika Fasihi Simulizi: Fanani, Hadhira, Wanyama, Binadamu, Mazimwi na Majitu (viumbe vya ajabu vyenye matendo ya kutisha kama vile macho mengi au kumeza kila kitu), Wahusika Vitu (mawe, miti, vibuyu), Mizimu (roho za waliokufa), na Miungu.